Baada ya kuridhishwa na usajili ambao umezingatia mapendekezo yake kwa asilimia 100, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi sasa amehamia kwenye benchi lake la ufundi akipendekeza kuongezwa kwa wataalam wawili muhimu
Nabi anataka mtaalam wa kusoma video za wapinzani pamoja na mtalaam wa lishe
Nabi amebainisha kuridhika na kazi nzuri inayofanywa na timu yake inayomsaidia kwenye benchi la ufundi lakini amehitaji watu hao kwa lengo la kuboresha zaidi.
"Hawa wasaidizi wangu wote niliokuwa nao nimewaambia viongozi nimeridhika na ufanisi wao, kuanzia Kaze (Cedric) na wote wengine waliosalia nataka kuendelea nao"
"Kuna watu zaidi tutawaongeza hapa kama uongozi utafanyia kazi kwa ufanisi, ukiangalia sasa sisi makocha ndio tumekuwa tukitafuta mikanda ya wapinzani na kuifanyia kazi.Tunahaja ya kuwa na mtu maalum wa kufanya hii kazi ambaye ana ubora kisha akaimaliza ataleta ripoti kwetu na sisi tunakwenda kufanyia kazi"
"Tunakwenda kwenye mashindano magumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika lazima uwe na mbinu za kisasa"
"Tuna mpishi wa chakula hapa lakini tunahitaji pia mtu wa lishe aliyesomea taaluma ya lishe kwa wachezaji ili tuweze kuwa salama zaidi eneo hilo," Nabi alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti