Afisa Mhamasishaji wa klabu ya Yanga Haji Manara amesema Kocha Nasreddine Nabi ni Mwananchi na hakuna yeyote anaweza kumn'goa katika klabu ya Yanga
Manara aliyesema hayo akijibu maswali ya Wanahabari waliohoji hatma ya Nabi baada ya kuibuliwa tetesi kuwa Simba walikuwa wakimnyemelea
"Nabi ni kocha wa Yanga na hakuna timu Tanzania inayoweza kumn'goa Yanga, hao wanaosema watamchukua hawana hela, kwanza walipe madeni ya mishahara ya wachezaji wao kabla ya kumfikiria Nabi," alisema Manara
Aidha akizungumza katika Mkutano huo na wanahabari, Manara amesema wamejipanga kufanya mambo makubwa zaidi kwenye wiki ya Mwananchi inayotarajiwa kufanyikwa mwanzoni mwa mwezi August 2022
Manara amesema katika wiki ya Mwananchi watashusha wachezaji kweli huku akitamba kuwa wiki hii wataanza kutambulisha mchezaji mmoja mmoja
Manara ameupongeza uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla kwa kazi kubwa waliyoifanya msimu huu ambao umekuwa na mafanikio makubwa
"Napenda kumpongeza sana Mwenyekiti wetu Dkt. Mshindo Msolla na Kamati yake ya Utendaji kwa kazi kubwa sana waliyoifanya, Nimekuwa kwenye michezo miaka mingi na kufanya kazi na ciongozi mbalimbali lakini Mwenyekiti wetu ni mtu mwenye busara na ana ukomavu mkubwa kwenye mambo ya mpira," alisema