Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema wanatambua mchango wa mshambuliaji Saido Ntibazonkiza hivyo watamualika kwenye sherehe za ubingwa apate kuvaa medali
Jana Yanga ilitangaza kuachana na Ntibazonkiza baada ya mkataba wake kumalizika
Bumbuli amesema uamuzi huo ulifikiwa baada ya makubaliano ya pande zote mbili yaani Yanga na Saido mwenyewe
"Kulikuwa na mazungumzo kati yetu Yanga na Saido juu ya kuongeza mkataba. Lakini mwishoni hatukuweza kufikia makubaliano. Sisi hatukukubaliana na matakwa ya Saido na yeye hakukubaliana na ofa tuliyokuwa tumempatia"
"Mkataba wake ulifikia tamati May 30, sasa kwa kuwa hatukukubaliana katika mazungumzo ya mkataba mpya, klabu haikuwa na la kufanya zaidi ya kumtakia kila la kheri katika maisha yake ya soka"
"Lakini Yanga inatambua mchango wake katika mwaka mmoja na nusu aliokuwa hapa. Msimu huu ameshiriki kikamilifu katika mapambano yetu ya kuwania ubingwa. Hakuna shaka tutamualika katika shamra shamra za ubingwa kwani ameshiriki katika mafanikio haya tunayokwenda kuyapata mwishoni mwa msimu huu," alisema Bumbuli
Mazungumzo ya mkataba mpya kati ya Yanga na Saido yalikwama baada ya Saido kuhitaji mkataba wa miaka miwili huku Yanga ikiwa tayari kumpa mwaka mmoja