Kocha msaidizi wa Yanga Cedrick Kaze amesema pointi moja waliyoipata dhidi ya Ruvu Shooting Jumanne ya Mei 4, 2022 haiwezi kuwaondoa katika mbio zao za kuwania ubingwa wa ligi kuu kwa msimu huu
Kaze amesema mchezo ulikuwa mgumu licha ya kutengeneza nafasi nyingi lakini hawakucheza vizuri kama kawaida yao.
"Hatuwezi kutafuta visingizo hii ni timu kubwa , lakini naamini mchezo wetu ujao dhidi Tanzania Prison tutajituma na kadri ya uwezo wetu tupate alama tatu'' amesema Kaze
Katika msimamo wa ligi kuu Yanga imefikisha alama 56 baada ya mechi 22 na kuiacha Simba kwa tofauti ya pointi 13 huku Ruvu Shooting wakibakia nafasi 13 wakiwa na pointi 22
Kimahesabu Yanga inahitaji kushinda michezo mitano kati ya nane iliyobaki ili kutwaa ubingwa msimu huu
Katika michezo nane iliyobaki, mitano itapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Michezo hiyo ni dhidi ya Prisons, Mbeya Kwanza, Coastal Union, Polisi Tanzania na Mtibwa Sugar wakati michezo iliyobaki nje ya jiji la Dar es salaam ni dhidi ya Biashara United, Dodoma Jiji na Mbeya City