Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema wamekamilisha maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari kuelekea mchezo huo, Kaze amesema wamewaandaa wachezaji kimwili na kiakili kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo
"Mechi za dabi ni maalumu na tofauti, takwimu haziamui sana sisi Yanga tunapaswa kujishusha na kusahau gap la pointi kwenye ligi na kuweka umakini wetu wote kwenye kutimiza malengo. Tumeshaandaa namna tunaenda kucheza mchezo huu na mtiririko wote, dakika 90 zitabaki kwa wachezaji kwani walimu maandalizi tunamaliza leo"
"Tumezungumza na kuwakumbusha wachezaji kuwa wanapaswa kupambana bila ya kufikiri yanayozungumzwa nje kwani katika mchezo wa dabi, takwimu na matokeo ya nyuma havina maana, ni dakika 90 zitakazoamua matokeo," alisema Kaze
Pamoja na kuchukua tahadhari kwa kuwaheshimu wapinzani wao, Kaze amesema Yanga haitabadili mfumo wake wa uchezaji
"Kesho hatutabadilika, tutacheza kama ambavyo tunacheza tangu mwanzo wa ligi, tutaongeza nidhamu ya kuzuia kwani tunatambua ubora wa wapinzani. Tutapiga pasi nyingi, mikimbio mingi na kushambulia sana huku tukijilinda kwa nidhamu"
Kaze pia alizungumzia hali ya majeruhi katika kikosi ambapo amesema watawakosa wachezaji wawili tu Chico Ushindi na Yacouba Songne ambaye anaendelea kuimarika baada ya kuwa nje kwa muda mrefu
"Chico alipata matatizo juzi na akapelekwa Hospitalini na Yacouba amekuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha aliyopata"
Naye mchezaji mwandamizi katika kikosi cha Yanga Deus Kaseke, amesema wanwaheshimu wapinzani wao Simba, ni timu nzuri lakini wao wamejipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 11 jioni