Mkurugenzi wa Maendeleo ya soka la Vijana Mwinyi Zahera amesema moja ya majukumu yake ni kuona Yanga inanufaika na wachezaji wake kutoka timu za vijana
Zahera anayesimamia timu za U17, U20 amesema tayari wamewaandaa vijana wengi akimtaja mshambuliaji Clement Francis kuwa yuko tayari kutumika kwenye kikosi cha kwanza
Katika mahojiano na Yanga TV, Zahera amemsifu Francis kuwa ni mshambuliaji mwenye sifa ambazo washambuliaji wa kisasa wanapaswa kuwa nazo
"Huyu ni straika hatari sana ambaye anaweza kutumika hata kwenye timu yetu ya wakubwa. Anatumia miguu yote na mzuri akiwa ndani ya box na hata nje. Ana kasi na msumbufu kwa walinzi. Nafikiri ni mchezaji ambaye atainufaisha Yanga," alisema Zahera
Mshambuliaji huyo kinda amesema yuko tayari kuitumikia timu ya wakubwa akiamini kwa kufuata maelekezo ya walimu wake, ataweza kufanikiwa
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla alisema kwa mkakati walioweka, wataanza kunufaika na wachezaji kutoka timu za vijana
"Tulimleta Mwinyi Zahera kwa kazi maalum kuhakikisha anatutengenezea timu zetu za vijana. Wachezaji ambao watakuwa tayari tutawapandisha moja kwa moja timu ya wakubwa kulingana na mahitaji yetu. Wale ambao wako tayari lakini tunaona hawatapata nafasi kwenye timu yetu ya wakubwa, tutawatoa kwa mkopo kwenda timu nyingine ili wakapate nafasi ya kucheza"
"Baada ya miaka michache tutakuwa na wachezaji wengi kwenye ligi, wapo ambao tutanufaika nao kwa maana ya kucheza katika timu yetu ya kwanza na wengine kuwauza kwa timu nyingine"