Mshambuliaji Fiston Mayele ni habari ya mjini kwa sasa hapa Tanzania. Ni kutokana na umahiri wake wa kufunga mabao katika kikosi cha Yanga akiongoza mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akiwa amefunga mabao 10
Mayele anachuana vikali na mshambuliaji wa Namungo Fc Reliants Lusajo ambaye pia amepachika mabao 10
Mayele ndiye mshambuliaji kiongozi katika safu ya ushambuliaji ya Yanga, akiwa katika kiwango cha juu sana kulinganisha na washindani wake Heritier Makambo na Yusufu Athumani ambaye alikaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha
Wakati Yacouba Songne akiendelea kuimarika, Kocha Mkuu wa Yanga anafikiria kuongeza mshambuliaji mwingine katika dirisha lijalo la usajili
Kama Yanga itatwaa ubingwa wa ligi kuu msimu ujao itashiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, ili kufanya vizuri katika michuano hiyo, inahitaji kuwa imara katika kila eneo
Kwa sasa Mayele haonekani kuwa na upinzani mkali katika nafasi yake jambo ambalo Nabi anasema halipaswi kuwa hivyo
"Nafurahi Mayele anafanya vizuri sana lakini kama ukichukua ubingwa unajipeleka katika eneo jingine ambalo unahitaji kuwa na ubora zaidi ya huu tulionao sasa"
"Tutahitaji mtu mwingine bora kama Mayele au zaidi, mimi naamini katika ushindani wa nafasi kwa wachezaji. Kwa sasa Mayele amebahatika kuwa na anguko la wenzake wapo ambao waliumia na wengine kutoanza vizuri," Nabi amenukuliwa na Mwanaspoti
"Nimeanza kutafuta mtu mzuri zaidi ingawa natambua sio kazi rahisi, sio kila wakati unaweza kubahatika kupata mshambuliaji kama Mayele, washambuliaji ni wachezaji ambao wako wachache sana wenye ubora"
"Kuna wakati katika mechi unatamani kuanza na washambuliaji wawili hili lazima tuanze kulifanyia kazi sasa ingawa kitu muhimu kutangulia sasa ni kuchukua ubingwa kwanza ili tubaki katika malengo yetu," aliongeza Nabi