Yanga imeanza vyema duru ya pili Ligi Kuu ya NBC wakishinda michezo yote miwili dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold
Wananchi wamecheza mechi 17, wameshinda michezo 14 na kutoka sare michezo mitatu yote ikiwa kwenye duru ya kwanza
Yanga imekusanya alama 45 ikiendelea kutamba kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nane dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili
Msimu huu Yanga imeonyesha kwa vitendo kuwa inautaka ubingwa wa ligi kuu baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo
Kocha Mkuu wa Yanga Nasredine Nabi amesema bado wana kazi ya kufanya kabla ya kuanza kufikiria ubingwa
Kazi hiyo ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo katika michezo 13 iliyobaki, matokeo hayo yatawahakikishia kutwaa ubingwa
Baada ya kufanya kikao na wachezaji na benchi la ufundi, Nabi amesema wameweka mwelekeo wao katika michezo iliyobaki
"Tunapaswa kuwa na mkakati wa kufanya vizuri katika kila mchezo unaokuja mbele yetu. Nimewaambia wachezaji hatupaswi kuangalia mwenendo ya timu nyingine, ili kujiwekea mazingira ya amani zaidi za kukusanya pointi nyingi na kuweka pengo kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa"
"Bahati nzuri wachezaji wote wameahidi kupambana na tumeanza duru la pili kwa kushinda michezo miwili ya mwanzo, imani yangu hali itakuwa hivyo hadi mwisho wa msimu na kutimiza malengo ya kubeba ubingwa wa ligi tulioukosa kwa misimu minne mfululizo," alisema Nabi
Mchezo unaofuata ni dhidi ya KMC ambao utapigwa March 19 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Yanga itacheza michezo saba mfululizo jijini Dar es salaam, kama Wananchi watashinda michezo yote basi watakuwa wamekaribia kutimiza lengo lao walilojiwekea msimu huu