Leo Yanga iko mkoani Mwanza ambapo majira ya saa kumi jioni watashuka dimba la CCM Kirumba kuikabili Geita Gold
Yanga inashuka uwanjani leo bila ya wachezaji wake watatu muhimu, Djuma Shabani (mgonjwa), Khalid Aucho na Saido Ntibazonkiza wakiwa majeruhi
Aucho amekuwa mchezaji muhimu katika eneo la kiungo, katika mechi za hivi karibuni akitengeneza ushirikiano wa aina yake na Salum Abubakar 'Sure Boy'
Habari njema kwa Yanga ni kuwa Sure Boy yupo fiti, akiwa katika kiwango bora sana na leo Feisal Salum 'Fei Toto' anarejea kikosini baada ya kumaliza adhabu ya kadi tatu za njano
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi huenda leo atamtumia Yannick Bangala katika eneo la kiungo sambamba na Sure Boy huku Feisal akisogea mbele
Ni wazi Dickson Job leo anarejea kwenye safu ya ulinzi ambapo anaweza kutumika katika nafasi ya ulinzi wa kati au mlinzi wa kulia
Kama Job atatumika kama mlinzi wa kulia, Zawadi Mauya ataanza sambamba na Sure Boy huku Bangala akiendelea kushirikiana na Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto katika safu ya ulinzi
Yassin Mustafa yuko timamu kiafya, Nabi huenda akamuanzisha leo ili amsogeze Farid Mussa nafasi aliyokuwa akicheza Saido
Lakini pia mawinga Denis Nkane na Dickson Ambundo wanaweza kutumika wote kama Nabi ataamua kuendelea kumtumia Farid katika safu ya ulinzi upande wa kushoto
Kinara wa mabao Fiston Mayele leo atakuwa na nafasi ya kuendeleza kasi yake ya kuzifumania nyavu akianza sambamba na Feisal
Mayele na Feisal wamehusika kwenye mabao 19 kati ya 25 yaliyofungwa na Yanga msimu huu
Wawili hao wanapoanza pamoja kwenye kikosi, tarajia kuona mmoja akifunga na mwingine akitoa pasi ya bao