Vinara wa ligi kuu ya NBC Yanga leo wako mkoani Mwanza kuwakabili Geita Gold katika mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba, saa kumi kamili jioni
Ni mchezo mwingine muhimu kwa Yanga kushinda ili kuhakikisha wanaendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi katika msimu ambao Wananchi wamepania kwelikweli kutwaa ubingwa
Hata hivyo hautakuwa mchezo mwepesi kutokana na ubora wa Geita Gold kwani walifanya usajili mkubwa dirisha dogo, usajili ambao umekiimarisha kikosi hicho mara dufu
Geita Gold wako katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 21, tofauti ya alama nne tu dhidi ya Namungo Fc inayoshika nafasi ya tatu
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi leo atalazimika kufanya mabadiliko ya lazima kwenye kikosi chake baada ya kuwakosa nyota wake muhimu kutokana na sababu mbalimbali
Mlinzi wa kulia Djuma Shaban atakosekana leo baada ya kuugua malaria, hali kama hiyo ikimkumba Chico Ushindi huku Khalid Aucho na Saido Ntibazonkiza wakiwa majeruhi
Hata hivyo baadhi ya wachezaji waliokosekana mechi zilizopita wanaweza kurejea leo baada ya kumaliza changamoto zilizokuwa zikiwakabili
Dickson Job na Feisal Salum watarejea kikosini baada ya kumaliza adhabu zilizokuwa zikiwakabili
Ni mchezo mgumu wa ugenini lakini sifa ya timu inayohitaji ubingwa ni pamoja na kupata matokeo katika michezo ya aina hii