Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema msimu huu wamejipanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu, watapambana kuhakikisha wanatimiza azma hiyo
Yanga tayari imecheza mechi 16 ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na alama 42, alama 11 zaidi ya watani zao Simba wanaoshika nafasi ya pili
Kumekuwa na dhana kuwa Yanga ni kawaida yao kuongoza ligi katika misimu ya hivi karibuni lakini kutwaa ubingwa inakuwa vigumu kwao
Ni dhana hiyo inayowapa imani hata mashabiki wa Simba ambao wanaamini timu yao itapangua alama zote walizoachwa na Yanga na kuweza kutetea taji la ligi kuu waliloshinda kwa misimu minne mfululizo
Mwakalebela amesema inawezekana katika misimu ya nyuma walifanya makosa wakashindwa kutwaa ubingwa licha ya kuongoza ligi lakini sio msimu huu, kwani wamejipanga kwelikweli kutimiza lengo lao
"Sisi tunautaka ubingwa, tuna dhamira ya dhati kabisa kushinda ubingwa msimu huu. Tunaonyesha kwa vitendo, sio benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na hata mashabiki ,sote tunazungumza jambo moja tu, tunataka ubingwa"
"Tunaongoza ligi kwa tofauti ya alama 11, hadi watufikie maana yake washinde mechi tatu na kutoka sare michezo miwili, wakati huo sisi tunafungwa tu, jambo ambalo wasilitarajie, Yanga hii ni moto mwingine," alitamba Mwakalebela
Wakati watani zao Simba wakitarajiwa kushuka uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya kesho Ijumaa kuikabili Biashara United, Yanga itasafiri jijini Mwanza kesho kuifuata Geita Gold kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu ambao utapigwa uwanja wa CCM Kirumba Jumapili