Baada ya kulikosa kombe la Mapinduzi, Yanga imepania kutwaa makombe yote mawili yaliyobaki ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema moto ambao wameuwasha hakuna wa kuuzima
Wananchi wako kileleni kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya watani zao Simba wenye alama 25 katika nafasi ya pili ya ligi hiyo, juzi waliitoa Mbao FC katika mchezo wa raundi ya 32 ya Kombe la FA uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya kushinda 1-0
Kutokana na mwenendo mzuri kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA, Bumbuli, amesema kwa bahati mbaya sana wamelikosa Kombe la Mapinduzi, lakini kwa sasa lengo lao ni kuchukua makombe yote mawili makubwa yaliyobaki na uhakika huo wanao kwa sababu wana kikosi cha wachezaji imara, benchi la ufundi lililo bora na viongozi thabiti.
"Mchezo dhidi ya Mbao Fc ulikuwa mzuri na watu wamefurahi sana, timu zote zilicheza mpira mzuri, ingawa Yanga tulicheza vizuri zaidi"
"Lengo letu mwanzo lilikuwa kuchukua makombe yote matatu, lakini moja tumeliachia, haya mawili tutahakikisha tunachukua na nina uhakika kwa hilo kwa sababu msimu huu tuna kikosi imara, benchi la ufundi bora na viongozi thabiti, tunaamini moto huu hakuna wa kuuzima," alitamba Bumbuli
Yanga tayari imerejea jijini Dar es salaam wakitokea Mwanza ambapo wameanza maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City ambao utapigwa Jumamosi, Februari 05 uwanja wa Benjamin Mkapa