Kocha wa makipa klabu ya Yanga Razak Siwa amesema mlinda Erick Johora anaonyesha umahiri wa kuzuia mikwaju ya penati mazoezini na ndio sababu walimpa nafasi kwenye mchezo dhidi ya Azam Fc kuelekea mikwaju ya penati
Katika mchezo huo wa nusu fainali kombe la Mapinduzi, Yanga iliondoshwa kwenye michuano hiyo kwa kufungwa mikwaju ya penati 9-8 Johora akishindwa kuokoa mkwaju wowote kama ilivyokuwa kwa kipa wa Azam Mathias Kigonya
Siwa amesema anaamini presha na hofu ya mchezo huo ndio iliyomfanya Johora ashindwe kuonyesha makali yake lakini ndiye mlinda lango mahiri zaidi linapokuja suala la mikwaju ya penati katika viwanja vya mazoezi
"Johora alijua kabisa kuwa ikifika penalti yeye analazimika kukaa golini kwani ndiye anafanya vizuri zaidi mazoezini. Kutokuwa na utimamu wa mwili kwasababu hachezi mechi sio sababu kubwa sana ila wakati mwingine kwenye hizi timu kunakuwa na presha pengine alipatwa na hilo ndio maana hakuonyesha ubora," alisema Siwa
Aidha Siwa raia wa Kenya amesema wao benchi la ufundi wamebeba lawama zote baada ya Yanga kuondoshwa kwenye michuano hiyo
"Kama makocha hatuwezi kukwepa lawama na Yanga ya sasa inahitaji matokeo ili kushinda makombe"
Yanga tayari imerejea jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union ambao utapigwa Januari 16 katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga