Yanga imetakata uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya baada ya kuichapa Mbeya Kwanza mabao 2-0 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 19
Yanga ilikuwa moto kwelikweli kwenye kipindi cha kwanza na pengine ingeweza kufunga mabao mengi kama wangetumia vyema nafasi walizotengeneza
Bao la kwanza liliwekwa kambani na Saido Ntibazonkiza kupitia mpira wa adhabu baada ya Feisal kufanyiwa madhambi nje kidogo ya 18
Wananchi wakaendelea kulisakama lango la Mbeya Kwanza na kufanikiwa kuweka kambani bao la pili kupitia kwa Fiston Mayele akipokea pasi murua kutoka kwa Feisal Salum aliyekuwa na kiwango bora sana leo
Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kama ilivyotarajiwa kwani Mbeya Kwanza walichukua mchezo wakitumia mipira mirefu
Hata hivyo safu ya ulinzi ya Yanga chini ya Bakari Nondo Mwamnyeto na Dickson Job pamoja na mlinda lango Djigui Diarra wanastahili pongezi kwa kazi kubwa walioifanya kupambana na mipira yote iliyokuwa ikitupwa angani na Mbeya Kwanza
Ni ushindi muhimu ambao unairejesha Yanga Dar ikiwa na alama zote tatu kuelekea mchezo dhidi ya watani zao Simba utakaopigwa Disemba 11




