Mashabiki wa Yanga wana kila sababu ya kutamba kwani timu yao imeimarika sana, pongezi nyingi kwa benchi la ufundi chini ya Kocha Nasreddine Nabi
Wananchi wameongeza dozi, walianza na moja moja, wakaja mbili mbili na jana wamefika tatu tatu katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1
Katika mchezo huo nahodha, beki kisiki Bakari Nondo Mwamnyeto alichangia katika upatikanaji wa bao la tatu akimpenyezea pasi Farid Mussa ambayo krosi yake ilijazwa kambani na Mukoko Tonombe kwa ustadi mkubwa
Mwanzoni mwa msimu kuna waliohoji uwezo wa Mwamnyeto kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, wengine wakisema hana uwezo mzuri wa kupiga pasi na kuanzisha mashambulizi kama ilivyo kwa Dickson Job na Yannick Bangala
Katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Azam Fc na Ruvu Shooting, Mwamnyeto amedhihirisha yeye ni 'master' wa kupiga pasi
Huyu mwamba amecheza dakika 180 pasipo kuharibu pasi yoyote. Amepiga jumla ya pasi 110
Pasi zake mbili zilipelekea Yanga kufunga mabao moja akimuwekea Feisal katika mchezo dhidi ya Azam Fc na nyingine akimuwekea Farid jana
Ile kauli ya kocha Nabi kuwa baada ya mwezi mmoja kikosi chake kitakuwa kimekamilika kwa asilimia 100% inadhihirisha kuna kazi inafanyika kwenye viwanja vya mazoezi
Wachezaji wa Yanga wanazidi kuimarika kwa mmoja mmoja na kwa timu pia