Yanga imeonyesha dhamira yake msimu huu kwa kuanza kwa kutwaa Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao SImba katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Bao la dakika ya 11 lililowekwa kambani na Fiston Mayele, limeihakikishia Yanga ushindi huo muhimu
Kilichowafurahisha wengi ni kiwango kilichoonyeshwa na timu na pia mchezaji mmoja mmoja
Yanga imedhihirisha kuwa msimu huu ina watu kwelikweli, wapinzani wajipange na moto huu wa Wananchi
Wakati Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Injinia Hersi Said akitambulisha usajili wa mlinda lango Djigui Diarra, alisema tumeleta kipa ambaye anaweza kudaka hata mishale
Wenyewe wamembatiza jina la 'Screen Protector', leo amedhihirisha yeye ni Protector kwelikweli
Lakini pia ameonyesha umahiri katika kuanzisha mashambulizi. Bao alilofunga Mayele lilianzia mguu kwake ambapo mpira wake mrefu ulitua mguuni kwa Farid Mussa aliyewaramba chenga walinzi wa Simba kabla ya kumtengenezea Mayele aliyepachika bao mahiri
Shabani Djuma, leo ameonyesha umahiri wake sio katika kushambulia tu. Uwepo wake ulimvuruga mlinzi Mohammed Hussein ambaye leo hakuonekana kuwa na madhara yoyote
Kibwana Shomari atawapa wakati mgumu sana walinzi wa kushoto Yassin Mustafa, David Bryson na Adeyum Saleh
Ameanza kuzoea kutumika kama mlinzi wa kushoto, yule Sakho na baadae Banda walishindwa kutamba mbele ya Kibwana
Bakari Nondo Mwamnyeto na Dickson Job wameendelea kufanya vizuri katika safu ya ulinzi lakini mbele yao wameletewa watu wawili wanaowalinda, Yannick Bangala na Khalid Aucho
Aucho na Bangala ni viungo wawili waliozima kabisa mipango ya Didier Gomes, kocha wa Simba
Bangala alifanya kazi zote chafu na wakati mwingine alipanda kuongeza nguvu kwenye mashambulizi wakati Aucho alikuwa mlainishaji wa maisha katika eneo la kiungo, leo alipiga pasi 42, pasi iliyopotea ni moja tu
Bado tabu iko palepale kwa walinzi wa pembeni, kwani huo moto wa Jesus Moloko ni zaidi ya Tuisila Kisinda!
Farid Mussa alikuwa 'supraise' kwenye kikosi kilichoanza leo lakini assisti yake ndio iliyoipa Yanga bao kupitia Mayele
Alikuwa na ushirikiano mzuri sana na Mayele katika safu ya ushambuliaji
Feisal Salum, huyu ndiye kiungo bora kwa Tanzania sasa, itoshe kusema hivyo
Yule Taddeo Lwanga alipaswa kutolewa mapema tu, kwani Feitoto alimvuruga kwelikweli leo
Kuna wachezaji kutoka Zanzibar, lakini pia kuna Fei Toto mmoja tu kutoka Visiwani!
Mayele amewaliza leo katika dabi yake ya kwanza. Msimu huu mashabiki wa Yanga watashingilia mabao mengi kutoka kwa mwamba huyu
Mshambuliaji hatari mwenye shabaha na macho ya kuliona lango!
Yeye na Heritier Makambo msimu huu watawafuta machozi mashabiki wa Yanga ambao timu yao imeteswa na changamoto katika eneo la ushambuliaji kwa misimu kadhaa iliyopita