Ni siku nyingine ya dabi ambapo mabingwa wa kihistoria Yanga watakuwa uwanjani kuwakabili watani zao Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi anahitaji kupata ushindi wake wa kwanza kwenye mcichezo ya mashindano msimu huu
Alipoteza mechi ya kirafiki wiki ya Mwananchi, akapoteza mechi mbili za ligi ya mabingwa, hivyo leo hakuna matokeo zaidi ya ushindi ambayo yatawapa furaha mashabiki wa Yanga
Yanga imekuwa na mwanzo mbaya kutokana na maandalizi hafifu. Lakini ni wazi sasa kikosi kimeimarika baada ya mazoezi mfululizo na kucheza mechi kadhaa za kirafiki pamoja na michezo miwili dhidi ya Rivers United
Mashabiki wanatarajia leo Nabi ataanza na kikosi imara ili kuhakikisha anapata matokeo mapema
Pengine yatashuhudiwa mabadiliko katika baadhi ya nafasi ambazo kuna wachezaji wamezoeleka katika kikosi chake
Walinzi wa pembeni Shabani Djuma, David Bryson leo wanaweza kuanza badala ya Kibwana Shomari na Adeyum Saleh
Pia eneo la kiungo Yannick Bangala na Khalid Aucho wanaweza kuanza badala ya Zawadi Mauya na Mukoko Tonombe ambaye anakosekana kwa kuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu
Mshambuliaji Fiston Mayele ndiye kinara wa mabao katika michezo ya kirafiki ambayo Yanga wamecheza Avic Town
Leo anaweza kuanza safu ya ushambuliaji sambamba na Heritier Makambo aliyetumika katika mechi zote za Kimataifa
Aidha mkongwe Saido Ntibazonkiza leo anaweza kuwa 'sapraizi' katika kikosi cha Yanga kama ilivyo kwa Deus Kaseke ambaye hata kama hataanza, anaweza kuwa na dakika zake katika mchezo huo
Pia wapo kina Yusufu Athumani, Yacouba Songne, Farid Mussa na wengine ambao wako tayari kupigania ushindi wa Yanga leo
Hakika ni mechi ambayo Wanayanga wanasubiri kushangilia ushindi baada ya dakika 90
Huu ni mchezo ambao Yanga inahitaji kushinda, kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya sita tangu ilipoanzishwa