Kocha Mkuu wa Yanga, Nasriddine Nabi amewataka mashabiki wa timu hiyo waache presha kwani msimu huu wana kikosi bora chenye uwezo wa kubeba mataji yote ya ndani na kuiwakilisha vyema Tanzania katika michuano ya kimataifa
Yanga ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Zanaco FC ya Zambia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwenye siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi, mchezo uliochezwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam juzi Jumapili
Akizungumza baada ya mchezo huo, Nabi alisema kupoteza mchezo ilikuwa ni sehemu ya kukijaribu kikosi chake ambacho hakijaanza maandalizi ya msimu ujao kikamilifu ingawa amefurahishwa na uwajibikaji wa wachezaji
"Mashabiki wetu hawapaswi kuwa na hofu, wajue wana timu nzuri msimu huu itakayoweza kubeba kila taji la ndani na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, matokeo ya mchezo wa Zanaco yasiwakatishe tamaa," Nabi aliliambia gazeti la Serikali la HabariLeo
Kocha huyo raia wa Tunisia alisema baada ya mechi ya Zanaco kupita, amepanga kuendelea na programu yake maalumu ambayo aliianza wakiwa nchini Morocco ili kukiimarisha kikosi chake katika kila idara kiweze kucheza soka la kuvutia na kupata maokeo katika mechi zote ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Septemba 12 watacheza na Rivers United ya Nigeria
Alisema mbali na vijana wake kuonekana bora kiufundi, lakini stamina pamoja na mifumo ya kiuchezaji imekuwa ni tatizo kwao, hivyo nalo amepanga kulifanyia kazi kwenye mazoezi yao ambayo yatakuwa ya wiki mbili kabla ya kukabiliana na Rivers United
"Tumesajili vizuri, imani yangu tutafanya vizuri cha msingi naomba wachezaji wetu waliokuwa timu za taifa wamalize majukumu yao haraka na waripoti kambini kwa wakati ili kuendelea na maandalizi yetu tukiwa kamili hakuna kitakachoshindikana"