Kocha wa zamani wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kikosi cha timu hiyo kilichosajiliwa msimu huu, ni bora zaidi katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita
Zahera ambaye alikuwa kocha wa Yanga msimu wa 2018/19, alikuwa mmoja wa wageni walioalikwa kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi uwanja wa Benjamin Mkapa hapo jana
Uongozi wa Yanga ulimpa Zahera heshima kwa kumualika kwenye Tamasha hilo kwa kutambua mchango wake na hamasa wakati akiwa kocha wa Yanga
Wiki ya Mwananchi ilianzishwa kama sehemu ya kuunga mkono juhudi alizoanzisha yeye kwa kuwashirikisha mashabiki wa Yanga kuichangia timu yao wakati ilipokuwa na hali ngumu ya kiuchumi
"Yanga wamesajili wachezaji wazuri nafikiri ndio timu bora waliyonayo katika kipindi cha misimu mitatu. Wamesajili wachezaji wakubwa ambao wamecheza matimu ya Taifa. Wachezaji wenye uzoefu wa kucheza Ligi ya Mabingwa na michuano mikubwa," alisema Zahera
"Mchezaji kama Yannick Bangala amecheza timu ya Taifa ya DR Congo ambayo ina wachezaji wengi wanaocheza Ulaya. Kupata nafasi ya kuitwa na kucheza Congo sio jambo dogo"
Baadhi ya wachezaji wenye uzoefu mkubwa waliosajiliwa katika kikosi cha Yanga ni pamoja na mlinda lango Djigui Diarra, Yannick Bangala, Heritier Makambo, Shabani Djuma, Fiston Mayele, Khalid Aucho na Jesus Moloko