Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema watahakikisha wanaunda kikosi imara ambacho kitawapa furaha mashabiki msimu ujao
Dk Msolla amewataka Wanachama na Mashabiki wa Yanga kutulia wakati viongozi wao wakiendelea kupambana kuiboresha timu
Amebainisha kuwa msimu uliomalizika waliweka malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kombe la FA lakini imekuwa bahati mbaya, hawakufanikiwa
Hata hivyo wanajivunia kuimarika kwa timu na sasa wakielekeza nguvu kwenye dirisha la usajili kufanya maboresho muhimu ili kuhakikisha msimu ujao wanaweza kuwa washindani sawasawa
"Malengo yetu ya kwanza ilikuwa ni kubeba mataji ya Ligi Kuu na Kombe la FA, lakini imeshindikana kwa kiwango kidogo sana tunajivunia uimara wa kikosi chetu lakini tunakwenda kwenye dirisha la usajili tumejipanga kukiboresha kikosi chetu kwa kusajili wachezaji ambao wataimarisha sehemu zenye mapungufu ili msimu ujao tuweze kutimiza ahadi yetu, " alisema Dk. Msolla
"Kabla ya msimu uliopita kumalizika tayari tulishaanza mchakato wa usajili kwa kushirikiana na kocha, na mpaka sasa kuna baadhi ya wachezaji tumemalizana nao"
"Tumekuwa makini kwenye usajili wa safari hii ndio maana tumefanya siri kutanganza wachezaji ambao tumemalizana nao lakini mchakato huo unakwenda vizuri na umekamilika kwa asilimia 90," aliongeza Dk Msolla
Baadhi ya wachezaji wapya wanatarajiwa kutangazwa kabla ya kuanza kwa michuano ya kombe la Kagame, Jumapili August 01 2021