Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi, leo ataingia katika mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kuwakabili Simba pasipo kuwa na presha yoyote
Nabi hawezi kuwa na presha kwa kuwa tayari 'ana watu' wa kucheza dabi. Watu hao walimdhihirishia Julai 03 walipopeleka ushindi Jangwani katika mchezo wa ligi kuu ambao wengi waliamini isingekuwa rahisi kwa Yanga kushinda
Nabi anao watu ambao akiwapa maelekezo wanatekeleza vile inavyotakikana na haishangazi kuona chini yake, Yanga imecheza mechi tisa mfululizo bila ya kupoteza
Tayari mkononi Nabi anacho kikosi chake cha ushindi akisubiri muda uwadie awatume pale uwanja wa Lake Tanganyika, wakafanye kazi ya kuchinja Mnyama
Miongoni mwa wachezaji waliosafiri Kigoma, ni kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza ambaye imeelezwa anaweza kuukosa mchezo leo baada ya kuumia mazoezini
Aidha kwenye kikosi chake, Nabi ana uamuzi wa kuwatumia nahodha Lamine Moro na Fiston Abdulrazak ambaye amerejea akiwa na 'mzuka' kuelekea mchezo huo
Kikosi cha Nabi hakitarajiwi kuwa na Mabadiliko makubwa, nafasi pekee ambayo huenda ikawa na mabadiliko ni eneo la ulinzi baada ya kurejea Moro
Hata hivyo Dickson Job amefanya vizuri katika michezo yote aliyoaminiwa, Nabi anaweza kuendelea nae leo
Huu ni mchezo muhimu zaidi kwa Yanga msimu huu, kwani matokeo ya ushindi yatawahakikishia Wananchi kutwaa taji la FA kwa mara ya pili tangu walipofanya hivyo msimu wa 2015/16 michuano hii ilipoanzishwa