Heritier Makambo ndiye mshambuliaji wa mwisho kuwapa furaha mashabiki wa Yanga misimu miwili nyuma, akiweka kambani mabao 18 kwenye ligi
Pamoja na kuwa alicheza Yanga katika kipindi kigumu cha 'njaa kali', Makambo aliifanya kazi yake vyema na haikushangaza baada ya msimu mmoja tu, akasajiliwa na Horoya Ac ya Guinea
Tangu ameondoka washambuliaji si chini ya watano wamesajiliwa lakini ni David Molinga pekee aliyemaliza msimu na mabao 11 wakati msimu huu Yacouba Songne amefunga mabao saba Yanga ikiwa imesalia na michezo mitano kukamilisha msimu
Ni takwimu zinazombeba Makambo kuwa mshambuliaji anayezungumziwa zaidi na mashabiki wakitamani arejeshwe
Wiki iliyopita Makambo alibainisha wazi kuwa hata yeye amekumbuka sana Tanzania, na zaidi amewakumbuka sana mashabiki wa Yanga
Makambo alijitengenezea ufalme Jangwani ndani ya msimu mmoja, imekuwa sio rahisi kutoka midomoni mwa mashabiki wa Yanga
Msimu uliopita GSM walijaribu kumsajili lakini haikuwezekana kwa kuwa Horoya walitaka kiasi kikubwa cha fedha
Makambo alisaini mkataba wa miaka mitatu alipojiunga na Horoya Ac, sasa amebaki na mkataba wa mwaka mmoja
Makambo 'aliwaheshimisha' Wananchi katika kipindi ambacho walikuwa na changamoto nyingi
Wengi wanaamini akirejea wakati huu wa 'neema' atafanya mambo makubwa zaidi
Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said amewataka mashabiki wa Yanga watulie, wasubiri wakati mwafaka, lakini ahadi imewekwa mezani kuwa watafanya usajili wa maana kwa ajili ya kuboresha maeneo yote yaliyobainika kuwa na mapungufu