Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, raia wa Senegal, Libasse Guèye, amefichua siri ya ubabe wa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27, akitaja maandalizi bora ya kimwili kuwa silaha kubwa ya mafanikio yao.
Simba imeendelea kutakata katika ligi hiyo baada ya kushinda mechi zote 11 za mwanzo mfululizo, ikijikita kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 33.
Akizungumza wakati wa Simba Media Day iliyofanyika jana, Gueye ameeleza kuwa kocha wa viungo pamoja na jopo la madaktari wa klabu hiyo wana mchango mkubwa katika mafanikio ambayo timu hiyo inayapata.
Nyota huyo amesema ushirikiano mzuri kati ya benchi la ufundi na idara ya matibabu umekuwa chachu ya kuwafanya wachezaji kuwa na utimamu wa mwili na kuendelea kucheza katika kiwango bora cha ushindani.
Ataja malengo makubwa Afrika
Guèye, ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu, amehusika katika mabao 11 kwenye mechi 11 za Ligi Kuu, akifunga mabao matatu na kutoa pasi nane za mabao.
Pamoja na mafanikio hayo, kiungo huyo amesema ndoto yake kubwa ni kuifikisha Simba mbali zaidi katika michuano ya kimataifa.
“Lengo langu kubwa na la klabu msimu huu ni kufika hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League),” amesema Guèye.
Kauli hiyo imekuja wakati Simba ikijiandaa kuvaana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika mchezo wa hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Asimama kidete kumtetea Doumbia
Katika hatua nyingine, Guèye amewataka mashabiki wa Simba kumpa sapoti kiungo Ibrahim Doumbia badala ya kumshambulia kupitia mitandao ya kijamii.
Amesisitiza kuwa Doumbia ni mpiganaji anayejitolea kwa ajili ya timu, hivyo anahitaji kuungwa mkono badala ya kuongezewa presha kutokana na ukosoaji mkali.
Aguswa na wimbo wa ‘Libasse Moto’
Aidha, nyota huyo wa Senegal ameeleza kufurahishwa na mapenzi makubwa anayoonyeshwa na mashabiki wa Simba, akitaja wimbo wa “Pige Kelele, Libasse Moto” kuwa moja ya vyanzo vya motisha kwake.
Amesema wimbo huo unaoimbwa majukwaani unampa hamasa ya kupambana na kufanya vizuri zaidi kila anapokanyaga nyasi.