Hatma ya ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) inatarajiwa kufahamika Jumanne, Novemba 24, 2026, wakati Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) itakapotoa uamuzi wa mwisho kuhusu sakata la fainali iliyozikutanisha Senegal na Morocco.
Kwa mujibu wa taarifa, CAS imeziarifu Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Morocco na Senegal kuwa uamuzi huo unaosubiriwa kwa hamu utatangazwa Jumanne mchana, ukitarajiwa kuweka mwisho wa mvutano wa kisheria kuhusu taifa linalostahili kutambuliwa kuwa bingwa wa Afrika.
NINI KILITOKEA KWENYE FAINALI?
Sakata hilo lilianzia Januari 18, 2026, wakati Senegal ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika mchezo wa fainali uliokwenda hadi muda wa nyongeza.
Hata hivyo, mchezo huo uligubikwa na utata mkubwa baada ya wachezaji wa Senegal kutoka uwanjani kwa takriban dakika 14 wakipinga uamuzi wa mwamuzi kuipa Morocco penalti katika dakika za mwisho za mchezo.
Licha ya Senegal kurejea uwanjani na hatimaye kupata ushindi, tukio hilo lilizua mjadala mkubwa kuhusu ukiukwaji wa kanuni za mashindano.
CAF YAIPA MOROCCO UBINGWA MEZANI
Mnamo Machi 17, 2026, Bodi ya Rufaa ya CAF ilitoa uamuzi uliobadilisha kabisa matokeo ya fainali hiyo.
Bodi hiyo iliamua kuwa Senegal ilikiuka kanuni kwa kuondoka uwanjani bila ruhusa, hivyo kuhesabiwa kuwa imepoteza mchezo kwa mabao 3-0. Uamuzi huo uliipa Morocco ushindi wa kikanuni pamoja na taji la AFCON 2025.
Hata hivyo, Senegal haikukubaliana na uamuzi huo.
SENEGAL YAKIMBILIA CAS KUTETEA TAJI
Mnamo Machi 25, 2026, Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) liliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), likipinga hatua ya CAF kuinyang'anya timu yake ushindi na ubingwa.
Senegal inataka uamuzi wa CAF ubatilishwe na ushindi wake wa bao 1-0 katika fainali urejeshwe, jambo ambalo lingeifanya kutambuliwa tena kama bingwa wa AFCON 2025.
JUMANNE NI SIKU YA MAAMUZI!
Sasa macho ya mashabiki wa soka barani Afrika yanaelekezwa CAS, ambako uamuzi unaotarajiwa kutolewa Jumanne unaweza kuhitimisha moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kisheria katika historia ya michuano ya AFCON.
Je, Senegal itarejeshewa ubingwa ilioupata uwanjani, au Morocco itaendelea kutambuliwa kuwa bingwa kwa ushindi wa mezani?