Drooo ya robo fainali ya UEFA Nations League msimu wa 2026/2027 imepangwa mjini Nyon, Uswisi, na kuibua michezo minne mikubwa itakayopigwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini mwezi Machi 2027.
Mabingwa wa dunia Spain watakutana na Ufaransa katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. Spain itaanza kwa kuwa mwenyeji wa mchezo wa kwanza kabla ya kusafiri kwenda Ufaransa kwa mchezo wa marudiano. Ufaransa chini ya kocha Zinedine Zidane itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya kikosi cha Luis de la Fuente kinachoongozwa na nyota Lamine Yamal.
England nayo itakutana na Norway katika pambano litakalowakutanisha washambuliaji hatari Harry Kane na Erling Haaland. England ilifuzu kwa hatua hiyo ikiwa kinara wa Kundi A3 baada ya kuifunga Spain mabao 3-2, huku Kane akimaliza hatua ya makundi akiwa mfungaji bora kwa mabao nane.
Norway ilipata nafasi ya kufuzu kwa ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Denmark, ambapo Haaland alifunga kwa penalti dakika ya 96 na kufikisha mabao sita kwenye michuano hiyo. Norway itakuwa mwenyeji wa mchezo wa kwanza mjini Oslo kabla ya kwenda Wembley kwa mchezo wa marudiano.
Katika mchezo mwingine, mabingwa watetezi Portugal watakutana na Netherlands inayonolewa na Xavi Hernandez. Portugal ilifanya vizuri katika hatua ya makundi chini ya kocha Jorge Jesus, huku Joao Felix akiwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri baada ya kufunga mabao matatu. Kwa upande wa Netherlands, Tijjani Reijnders alikuwa kinara wa mabao kwa kufunga manne.
Mchezo wa nne utazikutanisha Ubelgiji na Ujerumani katika pambano linalotarajiwa kuwa na mabao mengi. Ujerumani chini ya Jurgen Klopp ilitawala Kundi A2 na kuonyesha ubora kwa kuifunga Netherlands mabao 5-0, huku Florian Wirtz akifunga mabao manne katika hatua ya makundi. Ubelgiji ilifuzu baada ya kuifunga Italia mabao 4-1 katika mchezo wa mwisho wa kundi.
Michezo ya robo fainali itachezwa mwishoni mwa Machi 2027, huku timu zitakazoshinda zikifuzu kwa hatua ya nusu fainali itakayochezwa kati ya Juni 9 na 13, 2027.
Katika droo ya nusu fainali, mshindi kati ya Netherlands na Portugal atakutana na mshindi wa Spain na Ufaransa. Kwa upande mwingine, mshindi kati ya Ubelgiji na Ujerumani atakutana na mshindi wa Norway na England.