Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amekiri kuwa Simba SC ni timu kubwa na yenye ushindani wa hali ya juu, lakini amesisitiza kuwa kikosi chake kimejipanga kikamilifu kukabiliana na Wekundu hao wa Msimbazi katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa kesho Jumamosi, Novemba 21, kwenye Uwanja wa Isamuhyo, Mbweni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuelekea pambano hilo, Ahmad amesema maandalizi ya timu yake yamekwenda vizuri, huku akieleza kuwa wachezaji wake wameandaliwa kiakili na kisaikolojia ili kuhakikisha wanaingia uwanjani wakiwa tayari kupambana dhidi ya vinara hao wa ligi kuu.
Kocha huyo amekiri kuwa Simba si timu ya kubezwa kutokana na ukubwa wake na mafanikio iliyoyapata katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Hata hivyo, amesema ukubwa wa Simba hauwafanyi waingie uwanjani wakiwa na hofu, bali wanauchukulia mchezo huo kama fursa muhimu ya kupima uwezo wa kikosi chake na kujifunza zaidi kupitia ushindani wa kiwango cha juu.
Ahmad amesema kukutana na timu yenye uzoefu mkubwa kama Simba ni nafasi nzuri kwa wachezaji wake kuonyesha uwezo wao na kupambana kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Kwa upande wake, mchezaji wa JKT Tanzania, Jafar Maneno, amesema wachezaji wote wamejipanga kupambana kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo.
Maneno amesema lengo lao kubwa ni kupata alama tatu dhidi ya Simba, lakini iwapo watashindwa kufanikisha hilo, watahakikisha angalau wanaondoka uwanjani wakiwa na alama moja.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuwa na malengo yake, huku Simba ikihitaji kuendeleza mwenendo mzuri wa matokeo na JKT Tanzania ikisaka alama muhimu katika kampeni zake za Ligi Kuu ya NBC.