Winga raia wa Msumbiji, Luis Miquissone (31), ameanza rasmi mazoezi na kikosi cha Singida Black Stars leo Alhamisi, Novemba 19, 2026, ikiwa ni hatua inayotangulia kurejea kwake katika soka la Tanzania baada ya kuachana na klabu ya Al Ahli Benghazi ya Libya.
Miquissone ambaye anafahamika kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na historia yake ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa anaonekana kuwa karibu na kurejea kwenye ushindani wa ligi hiyo kupitia Singida Black Stars.
Winga huyo anatarajiwa kusaini mkataba wa kuitumikia Singida Black Stars katika dirisha dogo la usajili, baada ya kuanza kufanya mazoezi na kikosi hicho.
Ujio wake unatarajiwa kuongeza chaguo la wachezaji katika eneo la ushambuliaji la Singida Black Stars, huku uzoefu wake katika soka la ndani na nje ya nchi ukiwa miongoni mwa vitu vinavyoweza kuipa timu hiyo nguvu zaidi.