Kocha Mkuu wa Namungo FC, Juma Mgunda, amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi ya kuikabili Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa kesho Ijumaa, Novemba 20, 2026, kuanzia saa 12:30 jioni.
Mgunda amesema anatambua ukubwa wa upinzani anaokwenda kukutana nao, lakini amewaandaa vijana wake kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani kupata pointi zote tatu.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, kocha huyo amesema anatarajia ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuwa na uhitaji wa pointi katika ligi hiyo.
“Tuna mchezo kesho tunacheza na ndugu zetu kutoka Mbeya, Mbeya City, kwa hiyo naamini utakuwa ni mchezo wenye ushindani kutokana na mahitaji yanayofanana kwa sababu kila timu inatafuta alama,” amesema Mgunda.
“Kwa kutambua hayo tunaenda kupambana ili kuhakikisha alama zote tatu zinabaki hapa nyumbani kwa Wana Kusini, Namungo FC.”
Mgunda ameongeza kuwa maandalizi ya kikosi chake yamekamilika, huku akiwa na matumaini makubwa ya kuona wachezaji wake wakitimiza majukumu yao ipasavyo na kuibuka na ushindi.
“Maandalizi ya kucheza na timu nzuri yamekamilika, na kubwa zaidi ni kuwaombea vijana, kesho wakatimize wajibu wao kwa sababu utakuwa ni mchezo wenye upinzani mkubwa sana.
“Hivyo tumewaandaa vijana kwa ajili ya kushinda, na kwa baraka za Mwenyezi Mungu tunaamini tutaibuka washindi,” amesema.
Aidha, Mgunda ametoa wito kwa mashabiki wa Namungo na wakazi wa Ruangwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kutoa sapoti kwa kikosi hicho, akisisitiza umuhimu wao katika upatikanaji wa matokeo mazuri.
“Kwetu mashabiki wetu ni wachezaji wa 12, hivyo nachukua nafasi hii kuwaalika waje waungane na wachezaji ambao watakuwa ndani ya uwanja, hapo watakuwa wametimiza wajibu wao.
“Kwa mara nyingine niwaombe sana wana Ruangwa, wana Namungo waje kwa wingi kwa sababu ni sehemu ya matokeo ya timu yetu.”