Baada ya kusimama kupisha michezo ya kimataifa ya timu za taifa (FIFA Break), pazia la Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27 linatarajiwa kufunguliwa tena kesho Ijumaa, Novemba 20, 2026, kwa michezo mitatu kupigwa.
Mashabiki wa soka nchini watashuhudia jumla ya michezo sita ndani ya siku mbili, huku vigogo Simba, Yanga na Azam FC wakirejea katika harakati za kusaka pointi tatu muhimu.
Yanga itakuwa miongoni mwa timu zitakazoshuka dimbani kesho Ijumaa, ikitarajiwa kuvaana na Polisi Tanzania kuanzia saa 10:00 jioni.
Mchezo mwingine utazikutanisha Namungo na Mbeya City kuanzia saa 12:30 jioni, kabla ya Azam FC kumenyana na Singida Black Stars saa 3:00 usiku.
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, watarejea dimbani Jumamosi, Novemba 21, kuwakabili JKT Tanzania katika mchezo utakaopigwa kuanzia saa 12:30 jioni.
Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Steve Barker, kitakuwa na jukumu la kusaka ushindi ili kuendeleza mwenendo wake mzuri katika mashindano ya ndani.
Michezo mingine ya Jumamosi itazikutanisha Pamba Jiji na Coastal Union saa 10:00 jioni, huku Dodoma Jiji ikimenyana na Fountain Gate saa 3:00 usiku.