Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amefurahishwa na maendeleo ya wachezaji wake waliokuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha, ambao kwa sasa wameanza kurejea katika kikosi hicho.
Wachezaji hao ni Shomary Kapombe, Wilson Nangu, Abdurlazack Hamza na Vedastus Masinde, ambao kurejea kwao kunaongeza nguvu katika safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi.
Barker amekuwa akitumia michezo ya kirafiki kuwapa nafasi wachezaji hao ili kurejesha utimamu wao wa mwili na kuwaandaa kwa ajili ya michezo ya ushindani.
Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mashujaa uliochezwa Jumamosi jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita, nyota hao wote walipata nafasi ya kucheza.
Akizungumzia maendeleo ya wachezaji hao, Barker amebainisha kuwa benchi la ufundi litaendelea kuwapa dakika za kucheza taratibu bila kuharakisha kurejea kwao katika michezo ya ushindani.
Kocha huyo anataka kuhakikisha wachezaji hao wanakuwa katika hali nzuri ya utimamu wa mwili kabla ya kuanza kuwatumia kikamilifu katika majukumu mbalimbali ya kikosi chake.
Urejeo wa mastaa hao unakuja wakati muhimu kwa Simba, ambayo mbali na kuendelea kupambana katika mashindano ya ndani, inajiandaa na mikikimikiki ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.