Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeripotiwa kuhamishia jijini Dar es Salaam ofisi za uratibu wa maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, zilizokuwa Nairobi, Kenya. Hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa kitovu cha shughuli za uratibu wa mashindano hayo yatakayoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, Serikali ya Tanzania imeipatia CAF ofisi katika jengo lenye ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, lililopo eneo la Posta jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, sababu rasmi za kuhamishwa kwa ofisi hizo hazijawekwa wazi huku changamoto za kiutawala ndani ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) zikitajwa katika baadhi ya taarifa za habari kuwa huenda zimechangia uamuzi huo, ingawa hakuna uthibitisho rasmi unaounganisha suala hilo na mabadiliko hayo.
Uhamisho huo unajiri wakati maandalizi ya AFCON 2027 yakiendelea katika nchi hizo tatu, ambazo kwa kushirikiana na CAF zimeunda kamati ya pamoja ya usimamizi na uratibu wa mashindano hayo.