Uongozi wa klabu ya Simba, chini ya Mwenyekiti wake Murtaza Mangungu umetangaza kuwa uchaguzi wa viongozi wa klabu hiyo utafanyika Januari 30, 2027 ukiambatana na mkutano mkuu wa klabu hiyo.
Kupitia barua iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, Novemba 5, 2026, uongozi wa klabu hiyo umewajulisha wenyeviti wa matawi, wilaya na mikoa pamoja na wanachama wake kuwa mkutano huo utafanyika Jumamosi, Januari 30, 2027, kuanzia saa 3:00 asubuhi. Hata hivyo, eneo la kufanyika kwa mkutano huo halijatajwa katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa barua hiyo, mkutano umepangwa kwa kuzingatia Ibara ya 21(1) ya Katiba ya Simba ya mwaka 2018, iliyofanyiwa marekebisho Novemba 2025 na kusajiliwa Februari 18, 2026. Aidha, ajenda ya uchaguzi itasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa mujibu wa Ibara ya 20(6) na 22(i) za katiba hiyo.
Hata hivyo, kinachozua maswali zaidi ni tofauti ya tarehe zilizotajwa na pande hizo mbili. Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kiomoni Kibamba, alikuwa amesisitiza awali kuwa uchaguzi wa Simba unapaswa kufanyika kabla ya Januari 29, 2027, wakati uongozi wa klabu hiyo sasa umetangaza Januari 30, siku moja baada ya tarehe hiyo.