Mabingwa wa soka Tanzania bara, Yanga SC, wanatarajia kumtangaza kocha mpya wakati wowote baada ya kuthibitisha kuwa tayari amewasili nchini, huku taratibu za ndani za klabu hiyo zikisubiriwa kukamilika kabla ya utambulisho rasmi.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kocha huyo tayari yupo nchini na kinachosubiriwa kwa sasa ni kukamilika kwa taratibu za kiutawala kabla ya kutangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa kikosi hicho.
"Kocha tayari yupo nchini, kinachosubiriwa ni kukamilika kwa taratibu za ndani kisha tutamtambulisha," amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa endapo mambo yataenda kama yalivyopangwa, utambulisho wa kocha huyo unaweza kufanyika wakati wowote kuanzia leo.
"Kama mambo yataenda kama yalivyotarajiwa, kunaweza kumtambulisha wakati wowote ndani ya siku hizi mili," alisema Kamwe.
KOCHA MPYA KUKABIDHIWA PROGRAMU YA MAANDALIZI
Kuhusu maandalizi ya kikosi wakati huu ambao Ligi Kuu inatarajiwa kusimama kwa takribani wiki tatu kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Kamwe amesema klabu imeamua kumuachia kocha mpya jukumu la kupanga programu ya maandalizi ya timu.
Amesema uamuzi huo umetokana na umuhimu wa kumpa kocha nafasi ya kupanga mipango yake mapema, akizingatia kuwa baada ya mapumziko hayo Yanga itarejea katika michezo ya Ligi Kuu pamoja na kuendelea na majukumu yake katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hatua hiyo inatarajiwa kumpa kocha mpya nafasi ya kuifahamu vizuri timu, kutathmini mahitaji ya kikosi na kuweka mikakati ya kujiandaa na michezo ijayo.
RAMOVIC ATAJWA KUCHUKUA MIKOBA YA MNGQITHI
Wakati mashabiki wa Yanga wakisubiri kutangazwa kwa jina la kocha mpya, jina la kocha wa zamani wa klabu hiyo, Sead Ramovic, linatajwa kuwa ndiye mrithi wa Manqoba Mngqithi.
Ramovic si mgeni katika mazingira ya Yanga, jambo linalofanya taarifa za kurejea kwake kuendelea kuvuta hisia za mashabiki wa klabu hiyo.
Hata hivyo, hadi sasa uongozi wa Yanga haujatangaza rasmi jina la kocha huyo, hivyo macho na masikio ya mashabiki yanaelekezwa kwenye utambulisho unaosubiriwa.