Mashabiki wa Yanga huenda wakapata kile walichokuwa wakikitamani baada ya taarifa kueleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umefikia makubaliano ya kumrejesha kocha wa zamani, Sead Ramovic, kurithi mikoba ya Manqoba Mngqithi aliyefutwa kazi wiki iliyopita.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinaeleza kuwa makubaliano yamefikiwa na kinachosubiriwa ni hatua za mwisho kabla ya kocha huyo kutangazwa rasmi.
Inaelezwa kuwa Ramovic anaweza kuwasili nchini leo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kusaini mkataba na kuanza majukumu yake katika awamu ya pili ya kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Sead Ramovic si jina geni kwa mashabiki wa Yanga. Kocha huyo aliwahi kuitumikia klabu hiyo katika msimu wa 2024/25, akivutia sehemu ya mashabiki kupitia falsafa yake ya soka na namna alivyotaka kikosi chake kucheza.
Hata hivyo, safari yake ya kwanza Yanga haikudumu kwa muda mrefu baada ya kuondoka na kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria, ambayo ilivunja mkataba wake na Wananchi.
Uwezekano wa kurejea kwake sasa umeibua matumaini miongoni mwa mashabiki wanaoamini kuwa kocha huyo anaweza kuendeleza kazi aliyoianza kabla ya kuondoka.
Mashabiki walivyotaka Ramovic na Behlulovic warejee
Baada ya uongozi wa Yanga kuachana na Manqoba Mngqithi, mashabiki wengi walielekeza maoni yao kwenye mitandao ya kijamii wakimtaka Ramovic na kocha wa viungo Adnan Behlulovic.
Baadhi yao walimwomba Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, kuangalia uwezekano wa kuwarejesha makocha hao ili kuimarisha benchi la ufundi la klabu hiyo.
Iwapo atathibitishwa rasmi, Ramovic atakabiliwa na jukumu la kuijenga upya timu na kuhakikisha kikosi kinakuwa tayari kwa changamoto zinazokikabili katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Yanga ina malengo makubwa ya kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), hivyo kupata kocha mapema kutakuwa muhimu katika maandalizi ya kikosi, mbinu za mchezo na kujenga muunganiko kati ya wachezaji.
Falsafa yake inayotajwa na mashabiki kwa kauli ya “Gusa, achia, twende kwao,” ni miongoni mwa mambo yanayowafanya baadhi yao kutamani kurejea kwake.