Golikipa wa Mashujaa FC, Lameck Kanyonga, amesisitiza umuhimu wa magolikipa wazawa kupewa nafasi na kuaminiwa katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania, akieleza kuwa nchi ina makipa wengi wenye uwezo wa kushindana na magolikipa wa kigeni.
Kanyonga amesema changamoto kubwa inayowakabili magolikipa wazawa ni kukosa fursa za kutosha za kuonesha uwezo wao, hali inayowafanya washindwe kupata nafasi ya kuthibitisha ubora wao ndani ya ligi.
Ameeleza kuwa magolikipa wa Tanzania wanapaswa kupewa nafasi ya kucheza ili kuonesha uwezo wao, badala ya kuhukumiwa kabla hawajapata fursa ya kuonesha kile wanachoweza kufanya uwanjani.
“Tanzania tuna magolikipa wengi sana wazuri ambao wanaweza kushindana na wageni wanaokuja. Changamoto kubwa kwetu ni kutokupewa nafasi ya kuaminiwa,” amesema Kanyonga akizungumzia hali ya magolikipa wazawa katika soka la Tanzania.
Ameongeza kuwa mchezaji anapaswa kupewa nafasi ya kuthibitisha uwezo wake, na pale anaposhindwa kufanya vizuri ndipo tathmini ya uwezo wake inaweza kufanyika.
Kwa mujibu wa Kanyonga, kukosekana kwa nafasi hizo kunaweza pia kupunguza kujiamini kwa wachezaji wazawa, hivyo ametoa wito kwa klabu kuendelea kuwaamini na kuwapa fursa ya kushindana.