Mashabiki wa soka mkoani Tanga leo wanatarajia kushuhudia mtanange mkali wa Ligi Kuu ya NBC, wakati wenyeji Coastal Union watakaposhuka kwenye dimba lao la nyumbani la Mkwakwani kuwakaribisha Singida Black Stars FC.
Mchezo huo wa raundi ya nane uliopangwa kuanza saa 12:00 jioni za Afrika Mashariki, unazikutanisha timu mbili ambazo kila moja ikiwa na presha ya kusaka alama tatu muhimu baada ya kusuasua katika michezo yao iliyopita mwishoni mwa wiki.
Wenyeji Coastal Union, maarufu kama ‘Wagosi wa Kaya’, wanaingia uwanjani wakiwa na jeraha la kupoteza mchezo wao uliopita kwa kufungwa mabao 2-0 na Azam FC Oktoba 9 katika uwanja huo huo.
Kipigo hicho kimewafanya Wagosi kusalia na alama 7, hali inayomlazimu kocha mkuu wa timu hiyo kufanya marekebisho makubwa kwenye safu yake ya ulinzi na ushambuliaji ili kurejesha furaha kwa mashabiki wa nyumbani.
Kwa upande wa wageni, Singida Black Stars wanashuka dimbani wakiwa na tahadhari kubwa baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Dodoma Jiji FC katika mchezo wao uliopita uliopigwa mkoani Dodoma.
Singida BS ambao kwa sasa wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wakiwa na alama 10, wanahitaji ushindi leo ili kusogea juu kwenye msimamo.
Rekodi zawabeba wenyeji
Ukiangalia historia ya timu hizi zinapokutana Mkwakwani, rekodi zinawabeba zaidi Coastal Union. Katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu uliopigwa uwanjani hapo mwezi Mei mwaka huu, Coastal Union waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Vilevile, Wagosi wa Kaya waliondoa Singida Black Stars kwa mikwaju ya penalti 4-2 kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita baada ya sare ya 0-0.
Hata hivyo ni wazi mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa kwani Singida Black Stars wameonekana kuimarika zaidi msimu huu ukilinganisha na msimu uliyopita.