Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kati ya TRA United na Yanga SC, ambao awali ulipangwa kuchezwa Oktoba 13, sasa umehamishiwa Oktoba 24.
Mabadiliko hayo yanaifanya Yanga kupata ahueni kidogo ikiweka nguvu kwenye mechi za ligi ya mabingwa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya dhidi ya CFFA ya Madagascar.
Yanga itaanza kwa kuikaribisha CFFA katika mchezo wa kwanza utakaopigwa Oktoba 17 kwenye Uwanja wa Azam Complex, kabla ya kurudiana na timu hiyo Oktoba 21 katika uwanja huohuo.
Baada ya kumaliza majukumu yake ya kimataifa, Wananchi watasafiri kuelekea Arusha kuikabili TRA United Oktoba 24, katika mchezo wa ligi ambao sasa umepangiwa tarehe hiyo mpya.
Baada ya pambano hilo, kikosi cha Yanga kitarejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuikabili Mashujaa FC Oktoba 27, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa harakati zake za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC sasa wakishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nyuma ya watani zao Simba waliokaa kileleni baada ya ushindi wa mabao 2-1 waliopata juzi kwenye mchezo wa dabi ya Kariakoo uliopigwa uwanja wa Uhuru.