Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limemteua mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania, Ahmed Arajiga, kuwa mwamuzi wa kati katika mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).
Hatua hii inaendelea kuweka bayana kukua kwa imani ya shirikisho hilo kwa waamuzi kutoka nchini Tanzania katika hatua za juu za mashindano ya kimataifa.
Mchezo huo unaotarajiwa kupigwa Oktoba 17, 2026, utazikutanisha klabu ya Star Sport Academy ya Sierra Leone dhidi ya miamba ya soka ya Morocco, RS Berkane.
Katika mchezo huo utakaopigwa ugenini nchini Sierra Leone, Arajiga hatakuwa peke yake. CAF imeteua jopo zima la waamuzi wasaidizi kutoka Tanzania.
Waamuzi hao ni:
- Hamdani Said Ally – Mwamuzi Msaidizi Namba Moja (Line 1)
- Ally Ramadhani – Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili (Line 2)
- Nasir Siyah – Mwamuzi wa Akiba (Fourth Official)
Uteuzi huu unakuja wakati ambapo waamuzi wa Tanzania wamekuwa wakipata nafasi mbalimbali za kuchezesha mechi za kimataifa, jambo linalotajwa na wadau wa soka nchini kuwa ni matunda ya uwekezaji na mafunzo endelevu yanayotolewa na Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).