Shirikisho la Soka la Ghana (GFA) limefikia uamuzi wa kusitisha mkataba wa kocha mkuu wa Taifa hilo, Carlos Queiroz, baada ya Black Stars kuanza vibaya kampeni ya kufuzu AFCON 2027.
Ghana imepoteza michezo yake miwili ya kwanza katika Kundi C, ikifungwa mabao 2-0 na Ivory Coast ugenini kabla ya kupoteza tena nyumbani kwa mabao 4-2 dhidi ya Gambia. Matokeo hayo yameiacha Black Stars katika hali ngumu kwenye mbio za kufuzu michuano hiyo.
Kupitia taarifa yake, GFA imesema imefanya uamuzi huo kwa kuzingatia maslahi ya soka la Ghana, huku ikitambua mchango wa Queiroz katika kipindi chake cha uongozi. Kocha huyo alikuwa sehemu ya safari ya Ghana katika Kombe la Dunia 2026, ambako timu hiyo ilifikia hatua ya 32 bora.
Hata hivyo, mwanzo mbaya wa kampeni ya AFCON 2027 umefanya GFA kuchukua hatua ya kuachana na kocha huyo wa Kireno, ambaye sasa anaondoka katika benchi la Black Stars wakati timu ikiwa bado na kazi kubwa ya kupigania nafasi ya kufuzu.
Ghana sasa inatarajiwa kuanza mchakato wa kumpata kocha mpya atakayepewa jukumu la kuiongoza timu hiyo katika michezo inayofuata ya kufuzu AFCON 2027, mashindano yatakayofanyika kwa pamoja Tanzania, Kenya na Uganda.