Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameagiza kufanyika kwa tathmini ya mapendekezo ya kuongeza fedha zitakazogawiwa vyama vya soka wanachama wa FIFA kwa kipindi cha 2027 hadi 2030.
Hatua hiyo imekuja baada ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) pamoja na Shirikisho la Soka la Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) kuwasilisha pendekezo kwa FIFA la kutumia sehemu ya akiba yake kuongeza fedha zitakazokwenda kwa vyama wanachama.
Kwa mujibu wa pendekezo hilo, FIFA inatakiwa kutoa takribani Dola bilioni 2.1, sawa na karibu Sh5.6 trilioni, ambazo zitagawanywa kwa vyama vyake 211 vinavyounda shirikisho hilo.
Pendekezo hilo linataka kila chama cha soka mwanachama kupata angalau Dola milioni 10, sawa na takribani Sh27 bilioni, katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2027 hadi 2030.
UEFA na CONCACAF pia zimependekeza kufanyika kwa ukaguzi huru wa akiba ya FIFA, ambayo inakadiriwa kufikia karibu Dola bilioni 6, sawa na takribani Sh16 trilioni.
Mashirikisho hayo yameeleza kuwa iwapo FIFA itatoa Dola bilioni 2.1 kwa ajili ya mpango huo, bado shirikisho hilo litabaki na akiba inayozidi Dola bilioni 1.5, sawa na zaidi ya Sh4 trilioni.
Kwa mtazamo wa UEFA na CONCACAF, kiwango hicho cha fedha kitakachobaki hakitatarajiwa kuhatarisha uwezo wa FIFA kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kifedha.
Sasa Infantino ameagiza mapendekezo hayo yafanyiwe tathmini, hatua inayoweza kufungua mjadala mpana kuhusu namna mapato na rasilimali za FIFA zinavyoweza kugawanywa kwa vyama wanachama katika kipindi kijacho.
wapo mpango huo utaidhinishwa, vyama vya soka duniani vitakuwa na fursa ya kupata fedha zaidi kwa ajili ya kuendeleza soka, ikiwemo programu za maendeleo ya vipaji, miundombinu, ligi za ndani na shughuli nyingine za maendeleo ya mchezo.