Shabiki maarufu na mwanachama wa Young Africans Sports Club, Haji Omari Ramadhani Mpili, maarufu kama Mzee Mpili, amefariki dunia usiku wa Septemba 27, 2026, huko Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Yanga, Mzee Mpili alifariki katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri, alipokuwa akipatiwa matibabu. Taarifa kutoka kwa waliokuwa wakimfahamu zinaeleza kuwa alikuwa akisumbuliwa na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo maumivu ya mgongo na kiuno pamoja na matatizo yanayohusiana na uzee.
Mzee Mpili alikuwa akifahamika miongoni mwa mashabiki wa Yanga kwa mapenzi yake kwa klabu hiyo, huku kifo chake kikisababisha huzuni kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na familia kubwa ya wana-Yanga.
Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika leo Jumatatu, Septemba 28, 2026, saa 10:00 jioni katika Makaburi ya Msikiti Mkuu, Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.
Uongozi wa Yanga umetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wadau wa soka walioguswa na msiba huo, huku ukiwataka kuwa na subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Haji Omari Ramadhani Mpili mahali pema peponi na awape subira wafiwa. Amina.