Kocha Mkuu wa Gaborone United, Sean Connor, ameweka wazi kuwa timu yake haitaingia kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Yanga ikiwa na hofu, akiamini presha kubwa zaidi ipo upande wa wenyeji watakaokuwa wakicheza mbele ya mashabiki wao.
Gaborone United inatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya matokeo ya sare ya bao 1-1 mchezo wa kwanza, Connor amesema anatambua ukubwa wa kazi iliyo mbele yao, lakini anaamini kikosi chake kina uwezo wa kuipa Yanga wakati mgumu na kutafuta matokeo yatakayowasaidia kusonga mbele.
Kocha huyo amesema Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na mzigo mkubwa wa matarajio kutokana na kucheza nyumbani, huku mashabiki, vyombo vya habari na mazingira ya klabu yakiongeza presha kwa wenyeji.
Amesema Gaborone United inataka kuitumia hali hiyo kama nafasi ya kucheza bila mzigo mkubwa na kuilazimisha Yanga kufanya makosa.
Licha ya kuiona presha ikiwa upande wa Yanga, Connor hajaficha heshima yake kwa kikosi cha Wananchi.
Amesema wameutambua ubora wa Yanga, akitaja uwezo wa wachezaji wake, kasi yao pamoja na mchango wa benchi la ufundi kama mambo ambayo Gaborone United italazimika kuyadhibiti.