Klabu ya Simba SC inatajwa kukamilisha usajili wa wachezaji watatu wapya, huku uongozi wa Wekundu wa Msimbazi ukiharakisha kukamilisha mipango hiyo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili usiku wa leo Jumamosi, August 15 2026
Miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kutua Msimbazi ni mshambuliaji wa JKT Tanzania, Paul Peter Kasunda, mwenye umri wa miaka 27. Kasunda tayari amefikia makubaliano binafsi na Simba, huku klabu hiyo ikimalizia mazungumzo na JKT Tanzania kabla ya kumtambulisha rasmi.
Mshambuliaji huyo anatarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Simba baada ya kufanya vizuri msimu uliopita, ambapo aliifungia JKT Tanzania mabao nane.
Simba imeamua kumfuata Kasunda baada ya kushindikana kwa mpango wa kumsajili mshambuliaji Pape Abdou N’diaye, ambaye klabu yake haikuwa tayari kumuuza katika kipindi hiki.
Mbali na Kasunda, Simba tayari imekamilisha usajili wa Ibrahim Nindi, beki wa kati mwenye umri wa miaka 18, aliyekuwa akiitumikia KMC msimu uliopita. Nindi amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na KMC.
Nindi ana historia ya kuifahamu Simba, kwani alilelewa katika kikosi cha vijana cha Simba U20 kabla ya kujiunga na Mashujaa FC na baadaye KMC. Pia amewahi kuitumikia Singida Black Stars katika michuano ya CECAFA Kagame Cup.
Usajili wa Nindi unaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa Simba wa kujenga kikosi chenye vijana wenye uwezo wa kuitumikia klabu kwa muda mrefu.
Mchezaji mwingine ambaye tayari ametua Msimbazi ni Ismail Mgunda, aliyesajiliwa kutoka Mashujaa FC. Hivyo, Simba imekuwa ikifanya usajili wa haraka katika siku za mwisho za dirisha.