Kiungo wa Azam FC na timu ya taifa ya Tanzania, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’, ameongeza heshima nyingine kwenye rekodi yake baada ya kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka (MVP) wa Zanzibar kwa msimu wa 2025/26.
Fei Toto ameshinda tuzo hiyo katika Tuzo za ZFF/PBZ 2026, zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), akiwapiku baadhi ya nyota waliokuwa wakitajwa katika kinyang’anyiro hicho.
Katika ushindani huo, Fei Toto aliwashinda Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Mudathir Yahya wa Yanga, Suleiman Mbarouk wa JKU SC na Mohamed Mussa Salum (Mshujaa/Yanga), na hivyo kuibuka mshindi wa tuzo hiyo yenye heshima kubwa kwa soka la Zanzibar.
Tuzo hiyo ni mwendelezo w akutambua ubora wa Feisal Salum ambaye alionyesha kiwango bora katika msimu wa 2025/26 akiwa na Azam FC.
Takwimu za Ligi Kuu Bara zinaonyesha kuwa kiungo huyo alikuwa kinara wa ufungaji kwa kipindi kikubwa cha msimu, huku akifikisha mabao 14 na kutoa asisti nane, akihusika moja kwa moja katika mabao 22.