Kocha wa zamani wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi, anatarajiwa kutua jijini Casablanca kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mwisho za kujiunga na Raja Club Athletic (Raja CA).
Kwa mujibu wa taarifa, Nabi na Raja CA tayari wamefikia makubaliano ya awali kuhusu mkataba utakaoendelea hadi mwisho wa msimu ujao, huku masuala madogo ya kiutawala yakisalia kabla ya tangazo rasmi kutolewa.
Kocha huyo raia wa Tunisia atachukua nafasi ya Fadlu Davids kwenye benchi la ufundi la miamba hiyo ya Morocco. Raja imekuwa ikimfuatilia Nabi kwa muda mrefu kutokana na rekodi yake nzuri katika soka la Afrika na uzoefu wake mkubwa ndani ya ukanda wa Afrika Kaskazini.
Nabi ni jina linalofahamika sana kwa mashabiki wa soka Afrika Mashariki baada ya mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa kocha wa Yanga, ambapo aliiongoza klabu hiyo kutwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2023. Baadaye alihamia AS FAR ya Morocco kabla ya kujiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mwaka 2024.
Ingawa kipindi chake Kaizer Chiefs kilikumbwa na changamoto mbalimbali, Nabi aliweza kuiongoza timu hiyo kutwaa Nedbank Cup na kumaliza ukame wa miaka kadhaa bila taji, jambo lililoendelea kuimarisha hadhi yake kama mmoja wa makocha wanaoheshimika barani Afrika.



