Simba imekaa kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Simba inayonolewa na Kocha Robertinho Oliveira imeendelea kucheza kwa malengo ikikusanya alama tatu kutoka kila mchezo wa ligi
Prisons walitangulia kufunga bao la kuongoza kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Edward Balua
Hata hivyo bao hilo halikudumu kwani Simba ilirudisha na kuongeza la pili kabla ya mapumziko
Clatous Chama aliisawazishia Simba kwenye dakika ya 34 kabla ya nahodha John Bocco kufunga la pili dakika za majeruhi kuelekea mapumziko
Msumari wa mwisho uliwekwa kambani na Saido Ntibazonkiza kupitia mkwaju wa penati kwenye dakika ya 86 akiihakikishia Simba kuondoka na alama zote tatu
Yalikuwa matokeo muhimu kwa Simba kwani sasa Mnyama anakaa kilele mwa msimamo wa ligi na alama zake 12, alama mbili mbele ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 10
Aidha Singida FG nayo imepata ushindi wa kwanza msimu huu baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Manungu, Turiani
Bao pekee la Singida FG lilifungwa na Elvis Rupia kwenye akika ya 43. Singida FG imefikisha alama tano baada ya kushinda mechi moja, sare mbili na kupoteza mchezo mmoja