Kikosi cha Azam FC kimeingia kambini kujiandaa na mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), dhidi ya Simba utakaopigwa Mei 6, Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara
Azam Fc wamerejea mazoezini baada ya mapumziko ya muda mfupi ambapo kocha mkuu wa timu hiyo, Kally Ongala alisema amefurahishwa na urejeo wa nyota hao huku akiweka wazi wako na morali zuri
"Kila mmoja wetu yuko kwenye hali nzuri wakati tukijiandaa na mchezo huo mgumu na muhimu kwetu, hili ndilo kombe tunaloona tuna nafasi kubwa ya kulichukua hivyo lazima tujipange," alisema. Kally
Azam inakutana na Simba huku mchezo wao wa mwisho kucheza ulikuwa ni wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting na kuweza kushinda mabao 3-1, katika mechi iliyopigwa Aprili 22, Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Azam iliweza kuiondosha Mtibwa Sugar kwa kuifunga mabao 2-0 katika mchezo wa robo fainali ya (ASFC), huku kwa upande wa Simba ikitinga hatua hiyo kibabe kufuatia ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya Ihefu.