Mkufunzi wa Club Brugge Scott Parker amesema hana uhakika kama ataendelea kuwa kocha wa timu hiyo kufuatia kipigo cha Jumanne dhidi ya Benfica na kuwaondoa Wabelgiji hao kwenye Ligi ya Mabingwa.
Meneja huyo wa zamani wa Bournemouth na Fulham alikabiliwa na kibarua kigumu kupindua kipigo cha 2-0 kutoka kwa mechi ya kwanza.
Lakini pengine hangeweza kutarajia kichapo kigumu kama hicho kwani waliruhusu mabao matano nchini Ureno na kushindwa kwa jumla ya mabao 7-1.
Parker anakuwa meneja wa kwanza wa Uingereza kuruhusu mabao matano kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa huku Club Bruges ikiwa imeshinda michezo miwili pekee tangu kuteuliwa kwake mwishoni mwa Desemba
Parker amekubali mustakabali wake haupo mikononi mwake. Alipoulizwa kama bado atakuwa meneja Jumapili dhidi ya Standard Liege, aliiambia BT Sport:
"Sina uhakika. Sina udhibiti wa hilo. Nimeelewa kwa nini unaniuliza swali hilo na huenda limekuwa likinilenga mimi kwa wiki kadhaa sasa"
"Siwezi kudhibiti hilo kwa kweli. Siko katika nafasi hiyo kuelewa na unauliza labda mtu asiye sahihi. Nina nia ya dhati ya kujaribu kugeuza hili na hilo ndilo nitajaribu kufanya," alisema
Parker alitimuliwa na Bournemouth mwezi Agosti kufuatia kichapo cha 9-0 kutoka kwa Liverpool, mechi nne ndani ya msimu