Leo ni siku ya tatu tangu dirisha la kutolewa fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) lifunguliwe
Jumla ya wagombea tisa wamejitokeza kuchukua fomu, watano kati yao wakichukua fomu za kuwania urais wa TFF
Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo aliwataja wagombea ambao wamechukua fomu mpaka kufikia siku ya jana jioni
"Nafasi ya urais waliojitokeza hadi kufikia leo (jana) saa 10 jioni ni Deogratius Mutungi, Evans G. Mgeusa, Oscar Oscar, Wallace John Karia na Zahor Mohammed Haji.
"Kwa upande wa nafasi ya Kamati ya Utendaji ni Lameck, Nyambaya, Liston Katabazi na Michael Petro (Kanda namba 1- Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Mtwara na Pwani), mwingine ni Khalid Abdallah (Kanda namba 2- Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga)," Ndimbo alisema.
Karia ambaye anamaliza muda wake, yupo jijini Mwanza kwa majukumu yake ya kikazi ya shirikisho hilo, lakini juzi alichukuliwa fomu ya kutetea nafasi hiyo na Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba, Swedi Mkwabi, katika Ofisi za TFF jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa Oscar Oscar, ambaye ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa soka katika Kituo cha Redio EFM, baada ya kuchukua fomu jana, aliwaambia wanahabari wenzake kwamba ameamua kugombea nafasi hiyo ya urais kwa lengo la kuhakikisha maendeleo ya soka yanakwenda mbele zaidi.
"Nimeamua kuchukua fomu hii kwa sababu nina lengo la kuongoza mpira wa dunia, nimefikia uamuzi huu ninataka kuwa miongoni mwa watu wenye uamuzi wa kuhakikisha mpira wetu unasonga mbele," alisema Oscar.
Alisema moja ya uzoefu wake katika uongozi wa soka, kabla hajawa mchambuzi, aliwahi kufanya kazi akiwa miongoni mwa waajiriwa wa Klabu ya Azam kipindi ambacho timu hiyo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2014.
Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litafungwa keshokutwa Jumamosi, Juni 12 saa 10 jioni