Mchezo wa mkondo wa pili robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya Simba dhidi ya Kaizer Chiefs utapigwa keshokutwa Jumamosi uwanja wa Benjamin Mkapa
Huu ni mchezo ambao Simba inapaswa kupata ushindi wa angalau mabao 4-0 kuupeleka mchezo huo katika muda wa nyongeza au ushindi wa mabao 5-0 kwenda moja kwa moja nusu fainali
Hivyo ni mchezo ambao matokeo tofauti na ushindi wa kuanzia mabao manne hayatakuwa na maana yoyote
Ni mchezo ambao Simba itahitaji kushambulia kuanzia dakika ya kwanza na wakati huohuo wakihakikisha wanawazuia Kaizer Chiefs kufunga bao lolote
Kocha Didier Gomes amesema wamejipanga kimbinu kuhakikisha wanashinda mchezo huo
"Tunapaswa kupambana kiume, wachezaji, benchi la ufundi, viongozi pamoja na mashabiki tunatakiwa kujua kwenye mpira kila kitu kinawezekana na tunajiandaa kufanya hivyo"
"Nakubali hatukucheza vizuri kwenye mchezo wa kwanza hasa katika safu ya ulinzi lakini tunaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza mazoezini ili tusiyarudie tena," alisema Gomes.
Kwa mashabiki 10,000 watakaopata nafasi kuingia uwanjani, wanapaswa kuhamasisha wachezaji katika muda wote
Moja ya faida kubwa ambayo Simba wanaipata ni mashabiki kuruhusiwa kuingia uwanjani. Hii ni nafasi nyingine kwa wanamsimbazi kuongeza shauku ya kushinda katika mchezo huo
Ni mchezo ambao tunapaswa kushambulia.. kushambulia... kushambulia...